Tunaendelea na uchambuzi wa kundi H ambalo lina timu za Poland, Senegal, Colombia na Japan.

Wakati huu tuitazame timu ya taifa ya Senegal ambayo inashiriki fainali za kombe la dunia 2018 ikiwa sehemu ya mataifa matano kutoka Afrika yaliyofuzu kucheza fainali hizo, baada ya kufanya vizuri kwenye michezo ya kuwania tiketi ya kwenda nchini Urusi, hatua ya makundi.

Katika mchakato wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia kupitia ukanda wa bara la Afrika (CAF) Senegal ilipangwa kundi la D (Kundi La Nne) lililokua na timu za mataifa ya Burkina Faso, Cape Verde na Afrika kusini.

Michezo sita kwa timu shiriki kwenye kundi hilo ilishuhudia Senegal akimaliza na wingi wa alama (14), tofauti na wapinzani wake, hatua ambayo ililifanya taifa hilo la Afrika ya magharibi kufuzu fainali za kombe la dunia nchini Urusi.

Katika michezo sita ya kundi D, Senegal walifanikiwa kushinda michezo minne na kutoka sare mara mbili, jambo ambalo lilidhihirisha kikosi chao kipo vizuri, na huenda ubora huo ukaendelea watakapokua nchini Urusi wakipambana na Poland, Colombia na Japan kuanzia Juni 19.

Jina la utani la timu ya taifa ya Senegal: Les Lions de la Téranga (Lions of Teranga).

Mfumo: Kikosi cha Senegal hutumia mfumo wa 4-3-3.

Image result for Sadio Mané - senegalMchezaji Nyota: Sadio Mané (Liverpool)

Image result for M'Baye Niang - senegalMchezaji hatari: M’Baye Niang ( anacheza kwa mkopo Torino, akitokea AC Milan)

Image result for Cheikhou Kouyaté - senegalNahodha: Cheikhou Kouyaté (West Ham United)

Image result for Aliou CisséKocha: Aliou Cissé (42), raia wa Senegal.

Ushiriki: Senegal imeshiriki fainali za kombe la dunia mara moja (01). Mwaka 2002

Mafanikio: Robo fainali (2002)

 

Kuelekea 2018:

Kocha Aliou Cissé atakua na bahati ya kukiongoza kikosi cha Senegal kwa mara ya pili katika fainali za kombe la dunia tangu taifa hilo lenye watu zaidi ya 15,411,614, lilipoanza kushiriki fainali hizo.

Kwa mara ya kwanza Cisse’ alikiongoza kikosi cha Senegal  kama nahodha wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 2002 (Korea Kusini Na Japan) na sasa atakiongoza kikosi cha Senegal kama kocha mkuu.

Kocha Cisse’ anajivunia kuwa na kikosi imara ambacho kina uwezo wa kupambana na timu yoyote ya taifa duniani, kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa kisoka.

Asilimi kubwa ya wachezaji wa timu ya taifa ya Senegal wanacheza soka katika ligi za mataifa ya barani Ulaya, hivyo uzefu wa kucheza na wachezaji wa mataifa mengine kupitia ligi hizo, huenda ukawasaidia kuondoa hofu pindi watakapokua katika majukumu ya kusaka ubingwa wa dunia mwaka huu 2018.

Wachezaji kama M’Baye Niang, Keita Baldé na Sadio Mané wanaocheza nafasi ya ushambuliaji, wamekua wakichagiza mfumo unaotumiwa na kocha Cisse’ wa 4-3-3.

Senegal kwa mara ya kwanza waliposhiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2002, waliushangaza ulimwengu kwa kuwafunga mabingwa watetezi kwa wakati huo timu ya taifa ya Ufaransa na timu nyingine kama Uruguay waliyotoka nayo sare ya mabao matatu kwa matatu na baadae walifanya hivyo dhidi ya Denmark kwa kuambulia matokeo ya bao moja kwa moja.

Hatua ya mtoano walipangwa na Sweden na kuichabanga mabao mawili kwa moja, kabla ya kutolewa kwenye hatua ya robo fainali kwa kufungwa dhidi ya Uturuki bao moja kwa sifuri.

Dunia inasubiri kwa hamu ili kuona kama Senegal kama wataweza kurejea maajabu ya mwaka 2002, kupitia fainali za 2018 zitakazoanza nchini urusi Juni 14.

Senegal wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Poland, Uwanja wa Otkritie mjini Moscow Juni 19, kisha watapambana na Japan Juni 24, Uwanja wa Central mjini Yekaterinburg, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Colombia Juni 28,uwanja wa  Cosmos mjini Samara.

Kaa nasi, Dar24 kesho tutamulika timu nyingine na huu ni muendelezo hadi nyasi za Urusi zitakapoanza kupata joto la mitanange ya fainali hizo.

Hizi hapa sababu 7 za kutumia limao kila siku asubuhi
Wasimamishwa kazi kwa kuisababishia hasara serikali