Nchini Uganda Wilayani Bududa watu 34 wamefariki dunia mara baada ya kuangukiwa na maporomoko ya matope na mawe kutoka mlima wa Elgon yaliyosababishwa na mfululizo wa mvua za masika zinazonyesha katika maeneo ya milimani mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa shirika la msalaba mwekundu, Irene Nakasita amesema huenda wahanga zaidi wakagundulika wakati timu ya uokoaji ikiyafikia maeneo yote yaliyoathirika katika maeneo ya chini ya mlima Elgon kutokana kwamba watu wengi bado hawajapatikana.

Majumba yameharibiwa katika vijiji takribani vitatu na pia baadhi ya viungo vimepatikana kutoka kwenye matope.

Kamishna wa serikali anayehusika na masuala ya usimamizi wa shughuli za kudhibiti majanga katika eneo hilo, Martin Owor amesema kuna mto unaopita kwenye eneo hilo ambao ulivunjika kingo zake na kuharibu daraja na pia kusababisha hatari katika makaazi ya karibu na hapo.

Mnamo mwezi Machi mwaka 2010 takriban watu 100 walifariki katika tukio kama hilo la maporomoko ya matope katika eneo la Bududa na kila mwaka kunaripotiwa watu kujeruhiwa na kufariki wakati wa msimu wa mvua toka wakati huo Owor amefahamisha kwamba mpaka wakati huu tayari maiti za watu 31 zimeshapatikana na kutambuliwa kufuatia janga hili.

Ikumbukwe pia kwamba juhudi za serikali ya Uganda katika kipindi cha miaka kadhaa za kujaribu kuwahamisha wakaazi kutoka maeneo hayo ya chini ya milima hazijafanikiwa.Kadhalika imekuweko miito inayotolewa ya kuwataka watu wapande miti mingi zaidi katika maeneo hayo ya milimani.

 

Eden Hazard: Luca Modric anastahili Ballon d'Or 2018
'Drone' kuanza kutumika kusambaza dawa kwa wagonjwa majumbani